Wednesday 13 August 2014

Nafasi ya Vitendo Usemi katika kufanikisha Ulinganifu katika Tafsiri ya Kiswahili

Vitendo Usemi na Ulinganifu wa Maana katika Tafsiri

Tasinifu hii inatalii matumizi ya nadharia ya vitendo usemi katika kusuluhisha matatizo ya tafsiri ya Kiswahili. Msisitizo umatiliwa kwenye ngazi ya ilokusheni ambapo swali kuu linaloongooza utafiti wenyewe ni kwamba kutatokea nini iwapo tutahuruji nadharia ya VU na kuzitumia kama msingi wa kushughulikia tatizo la tafsiri ya Kiswahili? Msimamo wetu ni kwamba nadharia ya vitendo usemi inaweza kuwa faafu, lakini iwapo, mihimili yake itaeleweka na jinsi VU huibuliwa katika LL. Miundo ya kuibua VU ambavyo tumeainisha kwa kuzingatia kielelezo cha Searle imeshughulikiwa. Lengo letu ni kutambua kiwango  ambacho kwacho nadharia hii inaweza kusuluhisha tatizo la ulinganifu wa maana katika tafsiri.
Tasnifu itajengwa kwenye sura sita. Sura ya kwanza ni utangulizi unaofafanua suala la utafiti, madhumuni, ufafanuzi wa nadharia na njia za utafiti. Katika sura ya pili tunaeleza dhana mbalimbali ambazo zinahusu mada yetu ya utafiti kama vile nadharia ya VU pamoja na maswala ya kimsingi kuhusu nadharia ya tafsiri, ili kuijengea mada yetu mihimili thabiti ya kinadharia. Sura ya tatu, ya nne na ya tano ndizo kiini cha utafiti wetu ambazo zitahusu uchanganuzi na  uchambuzi wa VU mahususi kutoka vitabu tulivyoviteua. Katika sura ya tatu tunashughulikia VU na tafsiri kwa mkabala wa kimapokeo. Katika Sura ya nne tunashughulikia VU katika vitabu hivyo hivyo kwa kuzingatia lugha ya kifasihi. Sura ya tano tunajihusisha na VU kwa kuzingatia lugha ya ishara inayojitokeza katika vitabu hivyo hivyo. Kwenye sura ya sita tunashughulikia uchambuzi na uchanganuzi wa matokeo ya uchunguzi wetu na athari zake, yanayojitokeza kuhusu nadhariatete, ufaafu wa mwongozo wetu wa utafiti na hatimaye mapendekezo.
Istilahi muhimu: vitendo usemi, lokusheni, ilokusheni, palokusheni, Searle, tafsiri