Sunday 26 June 2011

VIPERA VYA HADITHI SIMULIZI

AINA ZA HADITHI

Hadithi zinaweza kuainishwa kwa misingi ama vipengele mbalimbali kutegemea sifa zake za ndani kama:

1.      Aina ya wahusika waliomo – Hekaya, hurafa, ngano ya mazimwi, mghani,
2.      Maudhui ya Hadithi – Mtanziko, kisasili, ngano ya usuli, soga, tarihi, shajara, kumbukumbu, kudhubahi, mchapo
3.      Urefu – mbazi
Mintaraafu ya hii tuna aina zifuatazo za hadithi

1.      Visasili

Ni hadithi za asili au vyanzo vya matukio au mambo fulani tata katika jamii kwa kuchunguza au kutoa visa vya chimbuko la matukio au mambo. Aghalabu huaminiwa na wanajamii ingawa huwa haina ushahidi wa kutosha. Visasili ni msingi wa kujieleza na kuyaeleza mazingira katika jamii na ni kielelezo kizuri cha historia. Asili ya mambo hutatiza na hivyo wanavisasili hutokea kutatua matatizo haya kihadithi. Hufungamana na historia na huakisi mtazamo wao kuhusu amali na asasi zao. Kwa jumla, huwakilisha imani na mtazamo wao kuhusu asili ya ulimwengu na mwenendo wake. Hutumiwa kuhalalisha baadhi ya mila.
Husimulia kuhusu matukio ya kiada: mianzo ya matendo yaliyozoeleka (unyago, jando, ndoa, tohara, maisha, kifo na imani mbalimbali). Pia hutoa utaratibu unaofuatwa kutekeleza desturi hizi. Huhusisha matukio yasiyotarajiwa katika maisha ya kawaida au hata ya miungu. Huonyesha juhudi za jamii kujaribu kuhifadhi maarifa fulani kujihusu. Si lazima kisasili kiwe na misingi ya kihistoria inayotambuliwa waziwazi.
Hufungamana pakubwa na ushairi simulizi: Liyongo (Waswahili), Mugasha na Kachenyanja (Wahaya).
Umuhimu
(a)    Hufafanua chanzo cha matukio mbalimbali katika jamii hiyo kuonyesha imani zake
(b)   Huwa sehemu muhimu ya historia ya jamii
(c)    Hutumbuiza na kuburudisha hadhira
(d)   Hutumika kuwasilisha baadhi ya mila na desturi
(e)   Kuonyesha imani za jamii kuhusu ulimwengu na maisha

2.       Ngano za Usuli

Ni ngano zinazotoa maelezo ya asili au chanzo cha jambo au hali fulani. Hujibu swali kwa nini hali fulani iko jinsi ilivyo. Kwa mfano asili ya kuku kuchakurachakura, kinyonga kubadilisha rangi, sungura kuwa na masikio marefu, fisi kuchechemea. Huchukuliwa na wanajamii kuwa ukweli na huonyesha uhusiano wa karibu sana kati ya binadamu na wanyama.

3.       Hekaya

Pia huitwa ngano za ayari. Ni hadithi inayotumia wahusika wajanja kuwasilisha ujumbe wake. Mhusika mjanja (ayari) hutumia ujanja wake kujitoa katika hali ngumu. Ayari hutumiwa kama funzo kwa binadamu dhidi ya kudanganyika kwa urahisi au kuonyesha madhara yawezayo kupatikana na kudanganyika huko
Sifa
(a)    Huwa na mhusika afanyiaye wengine ujanja (sungura, Abunwasi)
(b)   Ayari kutumia ujanja wake kuepuka hali fulani inayomshinda
(c)    Ujanja huo kufichua ujinga wa wahusika wengine (hasa wakubwa)
(d)   Hujengwa kwenye adili kuwa ukubwa si hoja, hoja ni akili
(e)   Ayari kutumia ujanja wake ujanja wake kupata nafasi kuwakejeli wengine au kujinufaisha

Umuhimu
(a)    Kuburudisha kupitia visa vyake vya kuchangamsha na kuchekesha
(b)   Kudhihirisha athari za ujinga na udanganyifu
(c)    Kuwasilisha funzo fulani kuhusu jinsi ya kupambana na hali fulani ngumu
(d)   Hutahadharisha dhidi ya kudanganyika haraka
(e)   Kutoa mafunzo mwafaka katika mazingira ya shaka na hila
(f)     Kufunza wanaodhulumiwa kwa kuonyesha umuhimu wa kutumia akili na hekima
(g)    Kufunza maadili ili watu waepuke ujanja
(h)   Kuwaokoa wanaodhulumiwa kwa kutumia akili
(i)      Kufunza kuhusu kutendea wengine wema
(j)     Kuchunguza suala la mgogoro kati ya uhalisia na udhanaidshi

4.       Hurafa

Pia huitwa ngano za wanyama. Ni hadithi yenye wahusika wanyama waliopewa sifa za binadamu kama kula, kulia, kuongea, kucheka na yote anayoyafanya binadamu. Wayama hawa huwakilisha binadamu
Kuna aina zifuatazo za hurafa:
(a)    Hurafa Tatizo
Huwa na tatizo au mtanziko fulani wa kimaadili. Hali hii hutokana na fumbo lililofichwa. Hutokana na mchezo wa maneno, matumizi ya mihusianisho na lugha ya utata
(b)   Hurafa za Kipembuzi
Huwa na hurafa kadha za maelezo ambazo zimetolewa mfululizo kwa namna ambapo kila moja iko wazi
(c)    Hurafa za Maelezo
Huwa na madai fulani yanayohusishwa na mfano. Hutoa maelezo au msingi wa hali fulani
Sifa
(a)    Wanyama wanaowakilisha binadamu
(b)   Matumizi ya tashhisi
(c)    Funzo kuwa wazi
(d)   Huwa na sifa zinazohimizwa (maadili, wema, upole, ukarimu) na zinazoshutumiwa (ulafi, ulevi, wizi, ukahaba)
Umuhimu
(a)    Kuelimisha wanajamii
(b)   Kurithisha maadili na mafunzo
(c)    Kuburudisha

5.       Mighani

Ni hadithi zinazohusu mashujaa walioishi au wanaoaminiwa kuishi na wanaosifiwa sana katika jamii. Aghalabu, mashujaa hawa waliongoza jamii katika vita fulani, ukombozi fulani au wakati fulani mugumu. Mashujaa hawa wa mighani huitwa majagina. Jagina hung’ang’a na hali ngumu unayosababishwa na maadui wanaoitwa majahili.
Ifuatayo ni mifano ya majagina kutoka jamii mbalimbali
Jagina
Jamii
Nchi
Luanda Magere
Luo
Kenya
Gor Mahia
Luo
Kenya
Fumo Liyongo
Pate (Waswahili)
Kenya
Koomenjue
Meru
Kenya
Wangu wa Makeri
Kikuyu
Kenya
Mekatilili
Giriama
Kenya
Sakagwa
Abagusii
Kenya
Otenyo
Abagusii
Kenya
Ombati
Abagusii
Kenya
Mwambo
Bukusu
Kenya
Vere Sango
Pokomo
Kenya
Koitalel arap Samoei
Nandi
Kenya
Nabongo Osundwa
Wanga (Luyha)
Kenya
Nyamgodho Ombare
Abasuba
Kenya
Lenana
Maasai
Kenya
Chege wa Kibiru
Kikuyu
Kenya
Masaku
Akamba
Kenya
Mwenda Mwea
Akamba
Kenya
Kinjekatile Ngwae
Wamatumbi
Tanzania
Mgasha
Wahaya
Tanzania
Mkamandume

Pemba
Shaka
Zulu
Afrika Kusini
Sundiata Keita
Mandika
Mali
Mwindo
Banyanga
Kongo (DRC)
Mfalme Arthur na Beowolf

Uingereza
Seigfried

Ujerumani
Sifa
(a)    Matumizi ya chuku kwa wingi
(b)   Jagina huwa na uwezo unaokiuka nguvu za kawaida (ukiamaumbile)
(c)    Jagina kupigania haki za wanyonge walio wengi
(d)   Jagina kufa kiajabu
(e)   Jagina mmoja kupigana na watu wengi mara nyingi akiibuka mshindi
(f)     Ukweli wa kihistoria waweza kubadilishwa kutokana na matumizi ya chuku
(g)    Hujengwa kwenye mgogoro baina ya jagina na jahili
(h)   Kuwepo kwa pande mbili zinazowakilisha mema na maovu ambapo jagina huwakilisha wema na jahili kuwakilisha maovu
Sifa za Jagina
(a)    Watu wema
(b)   Hupigania haki za wote au wengi
(c)    Kimo kisicho cha kawaida. Huwa wakubwa au wadogo kupindukia
(d)   Nguvu zao hutokana na siri fulani
(e)   Kifo chao huwa cha ajabu
Umuhimu wa Mighani
(a)    Huhifadhi historia ya jamii
(b)   Huburudisha
(c)    Huadilisha
(d)   Hueleza imani ya jamii kuhusu maumbile

6.       Ngano za Mazimwi

Ni hadithi zinazosimulia visa na maovu ya mazimwi. Zimwi ni kiumbe ambaye anayebuniwa tu na fikira za binadamu lakini si mnyama si binadamu. aghalabu ngano hizi hutumiwa kuonyesha ubaya wa maovu kama ulafi, tamaa, kinyongo, uongo, wizi, unafiki na uzembe. Mazimwi huishia kushindwa hasa na vijana wadogo na jamii kukombolewa.
Sifa za Mazimwi
(a)    Kuwa na akili za binadamu
(b)   Kuwa na sifa zinazokiuka mipaka ya binadamu kwa mfano vinywa viwili, pembe, jicho moja au manne
(c)    Kuweza kujibadili na kujipa sura ya ubinadamu hivyo kuwahadaa binadamu hata kuwaoa
(d)   Kuweza kuwaokoa wanaoteseka
(e)   Huwa nusu binadamu nusu shetani
(f)     Kutoaminika hata chembe
Umuhimu wa Ngano za Mazimwi
(a)    Kutahadharisha kuhusu hadaa za umbo la nje
(b)   Kuonya tusiwe na pupa bali tujaribu kujua jambo kabla ya kufungamana nalo

7.       Mtanziko

Ni hadithi ambazo wahusika wake hukumbwa na hali mbili ngumu ambapo wanalazimika kuteua moja kati yao. Hukusudiwa kukuza uwezo wa kufikiri na kusuluhisha mambo. 
Sifa
(a)    Hali mbili ngumu zinazohitaji uchaguzi wa moja
(b)   Tatizo kuu linalomkabili mhusika mkuu
(c)    Kuishia swali ambalo mtambaji anaiachia hadhira kujibu
Umuhimu
(a)    Kuipevusha hadhira kwa kuikuza na kuendeleza uwezo wao wa kuamua.
(b)   Huweza kuzua mjadala miongoni  wa wanajamii pamoja na kuukuza uwezo wa kushiriki majadala

8.       Istiara

Hii ni hadithi ambayo huwa na maana mbili –wazi na fiche.Maana wazi huificha maana ya  pili ambayokueleweka kwake huitaji ufahamu fulani wa muktadha  wa hadithi yenyewe.Wahusika na matukio yaliyomo huwa kama milinganisho na hali nyinginezo,yaani huwa kama stiari k.m.Hadithi ya binadamu kumhusu tembo kujistiri mkonga wake kisha anamfukuza binadamu kutoka nyumba   yake. Hiii ni sitiara ya Mwafrika kumruhusu mkoloni.

9.       Mbazi/Vigano

Ni hadithi zenye mafunzo kwa kutumia mifano; yaani zina wadhifa wa methali. Kimsingi, hadithi za aina hii hutolewa kama kielelezo hasa wakati wa maongezi au mazungumzo na hukusudiwa kumkanya na kumwelekeza, kuadhibu au hata kumfunza anayesikiliza.Mtambaji huwa anataka hadhira yake ijifunze   kutokana na hali au masaibu yaliyowafika wahusika.

10.   Mchapo/Kidahizo

Ni kisa kifupi kinachomhusu mtu au tukio fulani.Aghalabu wahusika wake huwa na maana nyingine ya ziada.Kutokana na kisa kisa hiki msomaji anapaswa kujifunza jambo fulani.Aghalabu hupachikwa kwenye hadithi kuu,hivi kwamba msimulizi huacha mkondo wa hadithi ili kueleza tukio fulani. Tunaweza kusema  utokajinje wa kidahizo.

11.   Ngano za Kichimbakazi/Kudhubahi

Ni ngano ambayo ni sehemu ya sanaa jadiiya na huchukua nafasi muhimu ya ngano.Ni hadithi    ambazo aghalabu hujifunza kwa matendo ya mhusika ambaye hukumbana na jasira za kila aina ambazo huhusisha matendo ya ukia- maumbile lakini mwishowe huishi maisha ya raha.Maajabu, uchawi, uganga na sihiri huchukua sehemu muhimu sana.Kisa cha sinderela ni mfano wa kidhubahi.Jasira(jasira)ni safari anayofanya mhusika inayohusisha   uvumbuzi fulani pamoja na kulabiliana na hali fulani ngumu.

12.   Soga

Ni hadithi ndogo zinazohusisha utani na ucheshi kwa kiasi fulani.Hudhamiriwa kuchekesha na kukejeli kwa kusema ukweli unaoumiza a.lakini unaofumbata ukali wa ukweli wenyewe. Hutambwa
katika mtiririko na hujengwa kwenye  tukio moja.
(a)    Huelekeza kwenye tabia inayofaa
(b)   Hukejeli matendo ya binadamu yasiyofaa
(c)    Huwasilisha mafunzo.
(d)   Huwa msingi mzuri wa burudani.
(e)   Huonyesha utani uliopo.
(f)     Njia nzuri ya kufufunza bila kutumia toni kali. 

13.   Tarihi


Ni hadithi ambazo husimulia au hujengwa kwenye matukio ya kihistoria.Matukio hayo yanaweza kuwa ya kweli au ya kubuni.Mifano maarufu ni Tarihi ya Pate na Tarihi ya Kilwa.Huguswa matukio maarufu ya utamaduni na utawala wa jamii.

14.   Kumbukumbu


Ni maelezo au hadithi za matukio yanayohusishwa na mtu fulani sana sana maisha yake.

15.   Shajara


Ni maelezo ya matukio kwa mujibu wa kutokea kwake (siku).Huwa ni hifadhi ya matukio kwa kutegemea siku.

Akungah o'Nyangeri