Mazishi yanapoisha, hofu ya
uchovuhumchochea mwana kutaka kuutua uzito wa huzuni aliyonayo ili
kuiridiha hali yake ya kawaida. Aliyefiwa hupawa motisha na wenzake kwa
kutomuuliza athari za kifo.
Teknohama imekuwa na mchango mkubwa
katika makuzi na maenezi na maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Imewawezesha wataalamu, wapenzi, walimu na wanafunzi wa lugha hii
kubadilishana maoni na mawazo kwa urahisi na wepesi. Uvumbuzi wa
mitandao ya kijamii umechangia mno kukiendeleza Kiswahili na kukivusha
mipaka ya uswahilini.mojawapo ya mitandao hii ni Facebook. Tangu
uvumbuzi wake mwaka 2004 kule Marekani, Facebook imejitokeza kuwa
maarufu miongoni mwa maashiki hawa wa Kiswahili. Nafasi ya utafiti wa
Facebook kukishughulikia Kiswahili imepanda sana ukilinganisha na
mitandao mingine ya kijamii ambayo hutumiwa na watumiaji wengine
duniani.
Waasisi wa Facebook walilenga kuwawezesha wanafunzi
kuwasiliana na kutambuana kila mmoja. Mtandao huu ulianzishwa kwa ajili
ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Harvard, lakini baadaye ulipanuka hadi
vyuo vingine vya maeneo ya Boston, Ivy League, na Stanford University.
Hatua kwa hatua ulifunguliwa katika vyuo vikuu vingine, na hata kufikia
kwa kila mtu umri wa miaka 13 na zaidi. Wanafunzi, waalimu na Wapenzi wa
Kiswahili kwa jumla ambao wamechangamkia mtanzao huu wameweza kutumia
huduma mbalimbali ambazo hutolewa nao kukipigisha Kiswahili hatua.
Wameunda kurasa na vikundi mbalimbali vya kushughulikia masuala
yanayohusu lugha hii. Vikundi ambavyo wameviunda ni pamoja na Umbuji na
Ulimbwende wa Lugha ya Kiswahili, Ramani ya Fasihi, Ramani ya Kiswahili
KBC Redio Taifa, Jamvi la Fasihi, Bahari ya Mashairi, Lahaja za
Kiswahili, Darasa la Tafsiri, Kisima cha Mashairi, Ushairi-Nikosoe
Nijenge, Ukumbe wa Waswahili na Utamaduni Wao, Ukumbi wa Mashairi na
vingine vingi.
Wanachama wa vikundi hivi kwa juma moja sasa
wamekuwa wakumuomboleza mshiriki mmaarufu na mkongwe zaidi kwenye kumbi
hizi. Omari Babu Marjan alijitokeza kuwa na mchango mkubwa kwenye
takribani vikundi hivi vyote.
Katika kumkumba marehemu kama
aliyechangia mno kundini, mdhibiti wa ukumbi wa Umbuji na Ulimbwende wa
Lugha ya Kiswahili wenye washiriki 21, 050 kwa sasa ametundika picha
yake kama picha ya kikundi chenyewe. Kwenye ukumbi huu ndiko rambirambi
nyingi zilikotumwa. Wapo waliotunga mashairi kuonesha kwamba mwendazake
alikuwa mshairi maarufi aliyewalea na kuwaelekeza. Wamemmiminia sifa za
ukarimu, upole, mwenye mlahaka mwema na nyinginezo nyingi. Kibwagizo cha
rambirambi zenyewe ni kwamba mchango wako ulioenziwa na wengi utawapita
huku akiliacha pengo kubwa ambalo ni vigumu kumpata atakayeliziba.
Isitoshe ukumbi huu ndio ulitumika kwa kiasi kikubwa kuyatangaza mauko
yake pamoja na mipango yote kuhusu mazishi.
Kumbi ambazo
hushughulikia mashairi nazo zimejaa tahalili za kishairi kumuenzi
mwalimu huyu. Maudhui ambayo yametawala tungo hizi ni kuhusu jinsi
mwalimu Omar alivyokuwa msitari wa mbele katika kuwalea, kuwaelekeza na
kuwahimiza watunzi chipukizi. Alichangia mashairi yasiyopungua mia
mbili. Isitoshe alikuwa na mazoea ya kusasisha hali yake kila mara
kishairi. Kupitia kwa masasisho yake wengi walijifunza kwamba katika
fasni ya utunzi, heri kuanza kwa ubeti mmoja kasha chipukizi akaendelea
kukua. Aliwahi kushiriki malumbano kadha, yakiwemo malumbano ya pete
ambayo walishiriki na rafiki yake tangu chuo kikuu Hassan Morowa. Ingawa
mwalimu alikuwa msomi, hakupenda kujinasibisha na tabaka la maulama.
Isitoshe kila mara watu walivyomrejelea kama bingwa, alikanusha hili na
kusema dama yeye mwanafunzi. Kwa mfano hapa ni chapisho lake kwenye
kikundi kinachoitwa Jamvi la Fasihi Juni 17, 2012.
“Mimi si gwiji wa
haya mambo. Nimechakura “maakaba” nikaangukiya tungo hizi tatu ambazo
ni mfano wa ulumbi. Kwangu mimi ulumbi mzuri ni wa tungo sampuli hii
maana zinajisimamia zenyewe. Ukisoma kila shairi kivyake linajisimamia
wala mtu hahitaji shairi la pili kuelewa maana. Al- akh Rashid Bakuli
alitunga tungo S’ENDEKEZE JINO BOVU na mimi nikafuatiliza MSI JITO
KWITWA TONGO. Al-akh Abubakar Hassan Mwamboga akatunga YONDA LIKOSAPO
BUNGO. Tungo zote hizo tatu hizo zinalingana vina na pia idadi ya beti.
Msomaji ambaye ni makini atajuwa moja kwa moja kwamba hizo tungo zina
uhusiano. Ulumbi mzuri ni huo wa kufumba bila kutajana. Nimeshasema mimi
si bingwa na pengine kuna watu walio na rai tafauti. Tunapojibu tungo
za watunzi wengine, tujitahidi kujibu kwa vina vyao ili kutiya ladha
kwenye hayo malumbano. Tusilalamike kwamba hayo ni masharti magumu.
Ikiwa mtu ni mtunzi, hayo anayaweza kama kucheza! Chembelecho Ustadh
Ahmad Nassir Juma Bhalo, Malenga wa Mvita:
“Kusota si kusangaa, na
kwenda si kusimama”. Kuna suala la maendeleo. Nadhani msanii bora ni
huyo aliye na nia ya kujiendeleza zaidi. Kwa hivyo watunzi wa tungo za
Kiswahili, tusione tumefika na kujipakazia ubingwa tusiokuwa nao. Hata
mwalimu ni mwanafunzi.
Mwalimu aliwahi kushiriki mijadala kuhusu
lugha ya Kiswahili ikiwemo kuhusu usuli wa Fumo Liyongo, Mashairi huru
ikiwa ni ya Kiswahili au la, Kiswahili Sanifu kipo au hakipo, Ngeli ya
neno maiti, Tafsiri ya neno Facebook na mijadala mingine kadha ambayo
wanachama wengi waliifuatilia na kuchangamshwa na mawazo yake ambayo
aliyajengwa kwa misingi thabiti. Wengi hupitia mijadala hiyo kila mara
ili kujikumbusha maswala muhimu kuhusu lugha ya Kiswahili. Mjadala
mwingineo aliwahi kuibua ambao ulikuza fani ya utunzi ni kuhusu uhuru wa
mtunzi. Mjadala wenyewe umechapishwa kwenye jamvi la Fasihi Januari 30,
2012. Kwa mantiki hii tunaweza kusema kwamba Omar alishangia katika
kukiweza Kiswahili Mtandaoni hivi kwamba yeyote anayesakura anaweza
kunufaika. Amekipa Kiswahili pumzi mpya kupitia mchango wake wa mijadala
pamoja na mashairi aliyoyatunga na kuyachapisha kumbini.
Kupitia
vikundi hivi wengi wamejiongezea marafiki pamoja na kuwasilisha maoni
yao kuhusu mada mbalimbali ambazo huibuliwa na wanachama. Omar aliwafaa
wengi na kifo chake kimewapokonya mtaalamu wa kutegemewa.