Sunday 26 June 2011

HADITHI SIMULIZI

HADITHI

Hadithi ni utungo wa kubuni unaosimuliwa kwa lugha nathari (mfululizo) wenye vito vya kufunza hekima, maadili namienendo au kuburudisha wanajamii.

Nadharia mbalimbali zimetolewa kuhusu vyanzo vya hdithi:
1.       Hadithi ilitokana na historia na mazingira ya jamii iliyozaa hadithi mbalimbali. Ngano zilizuka binadamu alipokuwa akipingana namazingira yake. Ngano hizo zilijazana. Visa-viini vilielezwa kwa  kutumia imani za kidini na kishirikina ,cha dunia na chanzo cha binadamu.
2.       Hadithi zilitokana na methali. Methali zote ni hadithi na hadithi zote ni methali. Visa vya hadithi ndivyo huzaa methali. Methali ni ufupisho wa hadithi.
3.       Mabadiliko ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni yalizua hadithi. Mabadiliko haya yalipoelezwa yalitoa hadithi.
4.       Shughuli  mbalimbali  za kijamii kama harusi, mazishi, jando, unyago hulimbua hadithi.

SIFA ZA HADITHI

1.       Huwa na mianzo maalumu
2.       Matumizi ya takriri kwa wingi ambapo maneno, nyimbo, sentensi au matukio hurudiwa kwa wingi
3.       Matumizi ya tamathali nyingi kama tashbihi, methali na balagha
4.       Miishio maalumu au kutajwa kwa funzo
5.       Matumizi ya tanzu nyingine kama nyimbo, ushairi, vitendawili, misemo, methali na mafumbo
6.       Wahusika mseto wanaoingiliana – wanyama, watu, miti, mawe n.k.
7.       Matumizi ya wakati uliopita
8.       Lugha cheshi na ya kutaharukisha
9.       Muundo rahisi kufuatika. Huwa na mwanzo, kati na mwisho uliowazi
10.   Masimulizi ya monolojia. Fanani husimulia yote yaliyomo hadithini
11.   Mandhari hayapewi nafasi kubwa, ila tu pale yanapohitajiwa kuongezea undani wa maudhui
12.   Uwezekano wa kubadilishwa kwa sehemu fulani kutegemea hadhira na mazingira
13.   Hutegemea mbinu za kidrama za mtambaji kama ishara-uso, miondoko au uigaji wa wahusika bapa wasiobadilika
14.   Matumizi ya virai-kiada kama vile hapo zamani za kale paliondokea

MUUNDO WA HADITHI

1.       Mwanzo

Hadithi huwa na kitangulizi. Utangulizi huu hukusudiwa kuteka nadhari ya hadhira na kuisisimua ari yao ili wajiandae kwa hadithi yenyewe. Huonyesha mwanzo wa hadithi; hutambulisha mtambaji; na huweka mpaka kati ya ulimwengu halisi na ule wa hadithi. Ifuatayo ni mifano ya vitangulizi
(a)    Msimulizi:   Paukwa!
Hadhira:       Pakawa!
Msimulizi:   Kaondokea chenjagaa
Kajenga nyumba kaka
Mwanangu mwanasiti vijino kama chikichi
Vya kujengea vikuta
Na vilango vya kupitia
(b)   Msimulizi:   Paukwa!
Hadhira:       Pakawa!
Msimulizi:   Sahani!
Hadhira:       Ya mchele
Msimulizi:   Giza!
Hadhira:       La mwizi!
Msimulizi:   Maziwa!
Hadhira:       Ya watoto wa nyayo!
(c)    Msimulizi:   Atokeani!
Hadhira:       Naam twaib!

2.       Mwili

Hii ndiyo sehemu inayobeba maudhui ya hadithi. Maudhui hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine kutegemea mazingira, dhima ya hadhiti na mahitaji ya jamii husika. Maudhui hujenga jamii na kuipa mwelekeo. Hadhiti zinaposimuliwa huipatia hadhira maadili yanayowasaidia kuyaendesha maisha yao na kuwafanya wafuate barabara msimamo au falsafa ya jamii. Pia huelimisha, huadibu na huonya jamii dhidi ya mwenendo usiokubalika. Mara nyingi hadithi husimulia watu wenye uchoyo, uzembe, wezi na sifa nyinginezo hasi.

3.       Kimalizio

Hapa kufa au kuishi raha mstarehe ndiyo miishio ya kawaida. Wakati mwingine watambaji humaliza tu kwa hadithi yangu imeishia hapo. Kimalizo huwa na majukumu yafuatayo:
(i)          Huashiria mwisho wa hadithi
(ii)          Huwa njia ya kupumzisha hadhira
(iii)          Kutanguliza shughuli inayofuata aghalabu mjadala au ufafanuzi wa hadithi

MTINDO WA HADITHI

Mtindo ni jinsi ya kujieleza katika hadithi. Kulingana na Buffon mtindo ni “mtu mwenyewe”. Hata hivyo inawezekana kukawa na mtindo wa wakati fulani au hata eneo fulani. Tunapochambua hadithi za Fasihi Simulizi, tunachunguza sifa kadha. Sifa hizi ni muhimu kama msingi wa kuielewa miundo ya hadithi hizo na viini vyake. Baadhi ya vipengele vya mtindo ni:
1.       Dhamira Na Maudhui
Dhanira ni wazo kuu au lengo la hadithi. Ni swala linalokuzwa na kuendelezwa na msuko pamoja na mahusiano ya wahusika mbalimbali. Maudhui ni jumla ya yaliyomo katika hadithi na yanayoibuka katika kuliendeleza wazo kuu (dhamira). Hujumuisha dhamira, falsafa (tasnifu), itikadi na msimamo
2.       Usisimuzi
Huu ni uwezo wa hadithi kuiteka hadhira. Kuna njia kadhaa za kufikia lengo hili – kuikuza taharuki vyema, mwingiliano mwema wa sifa nyingine za kimuundo na mbinu za utendaji anazozitumia fanani
3.       Urudiaji
Huweza kuwa vipengele vya muundo kama maneno, vishazi, virai, sentensi au wimbo. Pia unaweza kuwa urudiaji wa mawazi, fikira au maoni. Urudiaji ni muhimu katika kukuza kukumbbuka, kutia ladha na kusisitiza ujumbe
4.       Viliwazo
Kiliwazo ni sehemu inayokusudiwa kuituliza hadhira hasa katika hadithi ya kitanzia. Kiliwazo chaweza kuwa kifungu kilichojaa ucheshi au wimbo
5.       Matumizi ya Nyimbo
Nyimbo katika hadithi hutekeleza yafuatayo:
(a)    Kuonyesha na kusisitiza kiini cha hadithi
(b)   Kuishirikisha hadhira katika hadithi
(c)    Kuongeza uhai wa usimulizi kwa kupata hadhira tendi
(d)   Kuwapambanua wahusika wa hadithi
(e)   Kuondoa ukinaifu unaotokana na kutumia mtindo wa aina moja kwa muda mrefu
(f)     Kuizindua hadhira ambayo huenda ikawa imelala au kusinzia
(g)    Kama kiliwazo katika hadithi za kitanzia
6.       Tamathali za Semi
Haya ni matumizi ya lugha yenye mvuto ambapo neno au fungu la maneno hugeuzwa maana yake asilia na kuwa na maana nyingine. Tamathali hizi ni kama tashbihi, tashhisi, sitiari na tanakuzi
7.       Usambamba
Ni urudiaji wa muundo kupitia matokeo kadha kwa kuyasisitiza maswala makuu. Aidha ni kurudia dhamira ya hadithi. Unaweza kuwa wa kisintaksia, kisemantiki, kidhamira au kimuundo
8.       Usimulizi Hakiki/ Tunduizi
Huku ni kutoa maoni kunakofanywa na fanani kuihusu hadithi. Maoni yanaweza kuhusu wahusika au matukio fulani. Usimulizi tunduizi unaweza kuathiriwa kwa kiasi fulani na aina ya hadhira. Hadhira ya watoto huhitaji ufafanuzi mara kwa mara
9.       Utokaji kando
Ni mbinu ambayo kwayo mtambaji anatoka kando ya utambaji wake na kutoa maoni kuhusu hadithi moja kwa moja. Kuna utokaji kando wan je, ambao unatokana na sababu zilizo nje ya hadithi yenyewe kama vile hadhira ili kutosheleza mahitaji yao labda uchovu. Aidha kuna utokaji kanzo wa ndani, unaosanabishwa na nia ya kutoa maoni kuhusu tukio au kitu fulani katika hadithi yenyewe. Utokaji kando wa ndani unahusiana na usimulizi tunduizi na hutilia maanani hisia na mwitikio wa hadhira
10.   Hadhira
Hawa ni washiriki, watazamaji au wasikilizaji wa hadithi. Kuna aina mbili za hadhira – tuli  na  tendi. Hadhira tendi hushiriki katika uwasilishi wa hadithi kwa kuimba, kucheza, kupiga makofi na vifoli, kuitikia, kubadilisha wasimuliaji, kuuliza na kujibu maswali. Hadhira tuli haishiriki kwa njia yoyote bali inasikiliza tu
11.   Wahusika
Mhusika ni kiumbe wa kifasihi anayefanana au anayewakilisha binadamu. wahusika wa hadithi wanaweza kuwa binadamu, wanyama, miti, mimea, mawe au vifaa vilivyopewa sifa za binadamu. mapaka kati ya ulimwengu wa kawaida wa binadamu na wanyama haupo hadithini.
Katika baadhi ya hadithi, wanyama wakubwa huweza kushindwa na wanyama wadogo. Hii huwa ni njia ya kuwakejeli na kuwadhihaki wenye uwezo na nguvu lakini wasiotumia akili zao. Viumbe wakubwa na wa kudhaniwa kama mazimwi na majitu husawiriwa kama viumbe wanaoongozwa na tamaa kubwa, ulafi na uovu uliokithiri. Hii ni njia mojawapo ya kuakisi sifa zinazoonekana mbaya katika jamii.
Jamii mbalimbali huwa na wahusika tofauti wanaowakilisha sifa maalumu kwa mfano:
Jamii
Mhusika
Sifa
Afrika Mashariki
Sungura
Mwerevu, mjanja
Afrika Kati
Mbweha
Mwerevu, mjanja
Afrika Magharibi
Buibui
Mwerevu, mjanja
Jamii nyingi
Simba
Shujaa
Fisi
Tama, ulafi
Kobe
Mwenda pole, mwenye busara
Kinyonga
Kigeugeu, mwenda pole
Zimwi
Uovu
Njiwa
Amani, wokovu
Maji
Uhai
Ua
Maisha, furaha, upendo
12.   Msuko
Huu ni muundo wa hadithi, yaani mtukio ya hadithi yalivyopangwa kwanza mwanzo hadi mwisho yakifuatana. Kisababishi huandamwa na matokeo. Katika kitangulizi panazuka mvutano wa hadithi unaoendeleza mgogoro kati ya wahusika, harakati zao hadi kilele na hatimaye kusuluhishwa kwake au mpomoko. Huhusisha matendo ya nguli na jinsi yanavyowaathiri wahusika wengine.
Kaida za msuko ni ukubalifu, taharuki, mantiki, mshtukizo na mvuto
(a)    Ukubalifu. Hadithi inatarajiwa iaminishe au isadikishe katika misingi ya ulimwengu wa kiubinifu
(b)   Taharuki. Hamu kubwa ya hadhira kutaka kujua yatakayotokea katika hadithi
(c)    Mantiki. Matarajio ya kuwa matukio yaliyomo hadithini yanaonyesha mpatano unaokubalika kimanyiki katika ulimwengu wa kiubunifu
(d)   Mshtukizo. Ugumu wa kuyatabiri matukio au mwisho wa matukio fulani
(e)   Mvuto. Hii ni hali ya kupendezwa na kitu. Mvuto chanya hupatikana hadhira inapokuwa na hisia nzuri. Mvuto hasi ni pale inapochukizwa na kukerwa
Kuna aina mbalimbali ya misuko
(a)    Msuko Kinzani. Ni matukio ambayo kimsingi yamekusudiwa kufikia lengo au adili tofauti nay ale ya msuko mkuu. Inawezekana kuyaangalia matendo na malengo ya mhusika anayepingana na nguli kama msuko kinzani
(b)   Msuko kioo. Huhusisha mbinu rejeshi ambapo matukio hayafuatani kimpangilio. Kuna kurudi nyuma na labda hata kuenda mbele
(c)    Msuko linganuzi. Huelezea msuko ambamo matukio yake yanadhamiriwa kuwa kinyume nay ale ya msuko mkuu. Matendo na malengo ya mkinzani yanaweza kuwa msingi wa msuko linganuzi
(d)   Msuko mkuu. Ni msuko unaohusu hadithi kuu ambapo kuna hadithi kadhaa zenye msuko unaotambulika wazi
(e)   Msuko msago. Ni msuko wa moja kwa moja bila kuhusisha mbinu rejeshi
(f)     Msuko rudufu. Ni msuko zaidi ya mmoja unaopatikana katika kazi moja

UMUHIMU WA HADITHI

1.       Kuielekeza jamii kwa kufumbata mtazamo wa jamii pamoja na falsafa yake. Falsafa hii huwa kama kielekezi cha jamii
2.       Kuendeleza maadili ambayo huwa kama nguzo kuu kwa wanajamii. Kila hadithi kuwa na funzo maalumu linalotokana na mambo yanayopatikana katika hadithi
3.       Huonya, huadibu, huelimisha na hunasihi jamii. Hadithi huwa na wahusika wenye wasifu fulani unaowafanya kutumiwa kuelekeza kwenye sifa nzuri hasa katika ngano za mazimwi
4.       Hurithisha jamii thamani na amali muhimu
5.       Huburudisha hadhira hasa hekaya
6.       Hukuza ushirikiano na kuendeleza uhusiano uliopo baina ya wanajamii. Wakati wa kusimuliwa kwa hadithi, watu hujumuika pamoja hivyo kujenga msingi imara wa ushirikiano
7.       Hukuza kumbukizi ya watoto. Watoto huweza kukumbuka  mambo kutokana na tabia ya kusimuliwa hadithi na kutarajiwa wayasimulie kwa wenzao
8.       Kueleza maumbile na sababu za hali na matukio hasa ngano za usuli na visasili
9.       Kukuza maarifa na hekima
10.   Kueleza historia

UTAMBAJI WA HADITHI

Utambaji ni uwasilishaji wa hadithi kwa hadhira. Msimulizi wa hadithi ya Fasihi Simulizi huitwa fanani, mtambaji, mganaji au msimulizi. Katika jamii nyingi, fanani, aghalabu huwa watu wazima ingawa vijana pia huweza kutambiana.
Tuna aina mbalimbali za wasimulizi:
1.       Msimulizi Asopendeleo. Hapenyi kwenye akili za wahusika bali huyasimulia tu yanayoonekana. Jukumu la kuwafasiri wahusika linaachiwa hadhira
2.       Msimulizi Dukizi. Hukatiza usimulizi wake kwa nia ya kutoa mawazo fulani kuhusu mhusika, kitendo, tukio, hali au mandarin fulani. Wakati mwingine huweza kukatiza na kuingiza mawazo ambayo huenda hata yasihusiane na hadithi
3.       Msimulizi Fiche. Huwa ameficha. Hajitokezi kama msimulizi dukizi au wa kidrama. Kimsingi, huwasilisha matukio na hali bila ya kuingiza mtazamo wake au kuingilia kati ya hadithi kwa aina yoyote
4.       Msimulizi Horomo. Ni msimulizi, aghalabu wa nafsi ya tatu, atoaye maelezo tu na kuwaacha wahusika wa hadithi wazungumze wao wenyewe kwa wenyewe bila kuwaingilia
5.       Msimulizi wa Kidrama. Hutambulishwa na matumizi ya “mimi”. Husimulia tu bila kuingia kwenye akili za wahusika wengine
6.       Msimulizi Maizi. Ana uwezo wa kupenya katika akili na mioyo ya wahusika. Hutumia ufahamu wake mpana kufichua yote yanayohusiana na wahusika
7.       Msimulizi Mkengeushi. Anayakabili na kuyatathimini maswala kadha kwa njia isiyoelekea kupatana na mawazo na kaida za mtunzi
8.       Msimulizi Penyezi. Haridhiki tu na kusimulia bali hutoa maoni yake
9.       Msimulizi Tinde. Husimulia hadithi kwa kueleza hisi, mawazo na mambo ya mhhusika mmoja tu
10.   Msimulizi wa Kimsingi. Hupatikana katika hadithi zenye wasimulizi wawili au zaidi. Yule wa kwanza ndiye wa kimsingi
Utambaji wa hadithi huwa na sifa kadhaa zinazoutambulisha ili kutenga hadhithi ya Fasihi Simulizi kutoa kwa hadithi andishi. Sifa hizi huwa ni sehemu ya utamu ambao hatuwezi kuupata tusomapo kitabu. Sifa hizi ni:
1.       Usemi halisi wa moja kwa moja
2.       Michepuko yaani kanuni za pembeni au maoni ya mtambaji. Fanani anaiacha hadithi na kusema mambo ya pembeni kabla ya kurudi kuendelea tena kusimulia. Hii hunuiwa kuiliwaza hadhira
3.       Urudiaji wa maneno, vifungo au nyimbo
4.       Sauti igizi au za kimaelezi ili kufanikisha mawasiliano. Mtambaji hubadilisha lahani kutegemea hali.
5.       Matumizi ya viashirii mbalimbali kuukoleza usimulizi. Vishirii hivyo huwa ni kwa mikono, ishara za mwili, mkunjo wa uso, mchezesho wa macho au hata viungo vya mwili
6.       Matumizi ya wakati uliopo kihistoria. Utambajji huwa kwa wakati uliopita lakini huchanganya sifa za wakati uliopo ili kuhakikisha kuwa umbali uliopo kati ya hadhira na hadithi yenyewe umepunguzwa
7.       Uigaji wa sauti mbalimbali za wahusika na matendoyao kwa mfano kuchechemea kwa fisi, kupindapinda kwa nyoka na kuchupa kwa chura
8.       Mihusanisho ambapo mtambaji anaweza kurejelea dhana wanazozifahamu na matukio ya hadithi
9.       Kubadilisha muundo kwa kuongeza vitushi fulani, kurudia visa, kubadilisha msamiati, kurahisisha kisa au kutia ucheshi
10.   Mtuo wa kidrama ambapo fanani hutua kwa muda ili kuifanya hadhira kuwazia jambo anapotaka kusisitiza kitu, anapohitaji kupima upokezi wa hadhira au kujenga taharuki
11.   Matumizi ya meleba yanayochukuana na kisa. Maguo haya hutia uhai kisa na kuhakikisha hadhira itaguswa ipasavyo

SIFA ZA MTAMBAJI MWEMA

1.       Mchangamfu na mcheshi kwa hadhira yake. Ili kuwa mchangamfu lazima awe mbunifu ili kuwasilisha hadithi kwa njia inayoipa upya na upekee fulani
2.       Afahamuye hadhira. Ajue umri wao na mahitaji yao. Watoto, vijana au wazee huwa na matarajio tofauti tofauti. Aidha wanapendelea lugha tofauti
3.       Mjuzi wa lugha na utamaduni husika
4.       Mfaraguzi anayefahamu mbinu zifaazo za sanaa za maonyesho. Ufaraguzi ni uwezo wa kuunda, kugeuza na kuwasilisha kazi ya sanaa papo kwa papo bila kujifunga ka muundo asilia uliozoeleka. Mbinu hizi ni kama uigizaji, lahani na ishara
5.       Mwanasaikolojia anayefahamu tabia za binadamu na mikondo mbalimbali ya jamii. Anajua yanayomchukiza, yanayomkera, yanayomchangamsha, yanayomvutia na yanayompendeza
6.       Mwigizaji asiye na haya kutumia viungo vyake vya mwili kuwasilisha ujumbe anaoukusudia
7.       Akumbukaye vizuri
8.       Mtathimini wa yanayoendelea katika jamii ya sasa. Hivyo basi anaweza kuchangia kupitia tungo zake kueleza hali ya sasa ya mambo
9.       Abadilishaye kiimbo na kasi ya maneno yake kadiri ya ujumbe unaokusudiwa
10.   Asitaye maksuudi kuivuta nadhari ya hadhira ili kujenga taharuki
11.   Aelekezaye hadhira kushiriki kwa kutoa maoni, kuimba, kucheza, kupiga makofi au kujibu maswali
12.   Mlumbi hodari anayesikika na kuiongea lugha kwa njia inayoeleweka na hadhira yake

SABABU ZA KUBADILIKA KWA HADITHI

1.       Ufaraguzi wa fanani
2.       Mabadiliko ya wakati
3.       Mabadiliko ya mandhari
4.       Mabadiliko ya kizazi na falsafa za maisha
5.       Kusahaulika
6.       Kuwasilishwa vibaya
7.       Majilio ya elimu ya kigeni
8.       Utandawazi
9.       Maingiliano kati ya jamii mbalimbali
itaendelea kuhusu vipera vya hadithi

No comments:

Post a Comment